|
|
| This Month Newsletter |
|
|
 |
|
 |
 |
|
 |
 |
|
 |
|
Nyumbani
|
Taarifa ya Jumuiya ya Mwaka 1429/30 - 2009 |
|
|
|
|
Saturday, 13 March 2010 |
Yaliyomo;1. Utangulizi2. Jumuiya3. Kitengo cha Fedha4. Kamati ya Da’awah5. Madrasah6. Kinamama7. Mfuko wa Misiba8. Fundrising9. Uratibu shughuli za Jumuiya.10. Tovuti - Website11. Jengo12. Hitimisho
1. UtanguliziHatuna budi kumshukuru Allah Subhaanahu Wata’aala kwa kutuwezesha kuumaliza mwaka huu na huku Jumuiya yetu ikiendelea kuimarika kwa tawfiyq yake Subhaana.Kama ilivyo kawaida yetu kutoa ripoti ya mwaka ambayo huelezea kwa ujumla mafanikio, matatizo pamoja na mikakati ya jumuiya katika kuendesha harakati na kuhakikisha malengo tuliyojiwekea tumeweza kuyafikia na mikakati tutakayojipangia vipi tutaweza kuifikia.Ripoti itaelezea taarifa za vitengo vya Jumuiya pamoja na kuainisha mafanikio yaliyopatika na matatizo yaliyojitokeza na pia kujaribu kuweka malengo ya mwaka 2010 -1431 2. Uongozi wa JumuiyaKwa ujumla, uongozi wa Jumuiya uliweza kwa kiasi kikubwa kuitangaza Jumuiya hasa katika maeneo ya Northamptonshire na katika Jumuiya nyengine. Tumeweza kupata mialiko mbali mbali kutoka katika Jumuiya na asasi nyingine za kiserekali na kibinafsi kuhudhuria semina, mafunzo na warsha (workshops) za aina mbalimbali. Jumuiya iliweza kushiriki baadhi ya mialiko ambayo ilituhusu na ambayo tulikuwa na uwezo wa kushiriki.Uongozi pia ulihakikisha Jumuiya, licha ya kupita katika kipindi kigumu katika uongozi wake, iliweza kukabili changamoto zilizojitokeza bila ya kuathiri utendaji.Katika kipindi hiki Jumuiya ilishiriki katika Mikutano na semina zifuatazo;· Semina ya pamoja ya Jumuiya za Northamptonshire zinazomiliki majengo – Doddrige Cente· Semina za pamoja ya Jumuiya za Kiislamu za Northamptonshire zilizoandaliwa na Northampton Borough Council katika lengo la kutafuta suluhisho la suala la ugaidi – Violent extremism- Doddrige Centre/Fish Street· Mikutano ya pamoja ya Jumuiya za Kiislamu pamoja na Polisi katika kuunda chombo cha kuwasimamia Waislamu – Fish Street· Tulikuwa na vikao tofauti na CEMC - Council of Ethnic Minority wakati wa kuhangaikia suala la Appeal - Rufaa na kukajengwa uhusiano wa kuweza kutupa ushauri na misaada mengine tukihitajia – Northampton College Lower mounts.· Tuliwahi kushiriki kikao kilichoitishwa na Northamptonshire Muslim Council katika kuangalia njia gani za kukirudisha chombo hiki ambacho nasi tulikuwa miongoni mwa waasisi kilipoanzishwa 2006 - Somali Forum· Akinamama waliweza kushiriki katika Mkutano wa Forum ya Polisi ambayo nayo ilikuwa na na lengo la kuangalia vipi wataweza kujua matatizo ya akinamama na jinsi wataweza kuwasaidia.- Derngate· Tuliweza kuwasiliana na Ron Frater - aliyekuwa mkuu wa Community Police katika masuala mbali mbali yanayohusiana na Jumuiya.· Tuliweza kuhudhuria mkutano uliotayarishwa na BME (Black and Minority Ethnic Groups) Network is specialist strategic infrastructure organization which provides the framework and leadership to help people from different backgrounds to come together; supporting people to contribute to social and economic regeneration of Northamptonshire (Northampton College Lower Mount)· Tukishirikiana na CEMC tulihudhuria kikao cha kuomba Fund - London, kutoka Volunteering England· Tukishirikiana na CEMC tuliweza kuomba Grass roots fund kutoka WNDC kwa ajili ya Jumuiya bila mafanikio.· Jumuiya pia imeomba funding kutoka Northampton Borough Council chini ya partnership grant 2010. Bado hatajajibiwa kama tumefanikiwa au vyenginevyo. Maamuzi yatatolewa mwishoni mwa mwezi March 2010.Kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo tulionao na ukizingatia nafsi za kujitolea kwa wanachama wa Al-Iman si za kutosha kuweza kufanya kila tunalolihitaji, tunaweza kusema kuwa tumepiga hatua nzuri kimaendeleo ukilinganisha na miaka iliyopita. 3. Kitengo Cha Fedha Litengo cha Fedha kinasimamia mahesabu, matumizi pamoja na mapato na kinaendesha akaunti nne za Jumuiya, Akaunti ya Madrasah. Akaunti ya Misiba, Akaunti ya Jengo na Akaunti mama.Kwa ujumla kitengo cha fedha kwa mwaka kimeendelea vizuri bila ya matatizo yoyote makubwa ya kimsingi, mahesabu yote yalikwenda vizuri isipokuwa tu kwa matatizo madogo madogo ya kawaida 3.1 Mafanikio;· Ufuatiliaji wa kuhakikisha mahesabu yanakwenda ipasavyo na umeridhisha.· Udhibiti wa uingizaji na utoaji wa pesa ni wa kuridhisha.· Mashirikiano kati ya vitengo, uongozi katika masuala ya malipo na utoaji wa hundi umeongezeka kulinganisha na miaka ya nyuma, lakini jitihada zaidi zinahitajika.· Yamepatikana mafanikio ya kuridhisha japo si makubwa katika shughuli na matukio mbalimbali ya kutunisha fedha, ambapo mfuko wa Jumuiya uliweza kuongezeka na kusaidia kuendesha shughuli mbalimbali. 3.2 Matatizo· Jumuiya imefikia hatua ya kuwa na bajeti yake maalum ili kuweza kudhibiti matumizi yake, kwani kuna wakati mahitaji yanakuwa makubwa zaidi kuliko uwezo wa Jumuiya.· Uongozi wa kitengo cha fedha kwa kipindi kirefu zaidi ya miezi 12 umekuwa si mzuri. Mshika fedha mkuu amekuwa na muda mdogo sana wa kushughulikia shughuli za fedha na hivyo kuathiri utendaji mkuu wa kitengo kwa ujumla.· Pamoja na kuwa makusanyo na mahesabu yote yamewasilishwa kikamilifu, lakini kumekuwa na ucheleweshaji wa kukabidhi makusanyo kutoka vitengo vingine kama Madrasah na misiba.· Baadhi ya vitengo vya Jumuiya kama Fund raising vinahitajika kuwa na mfumo maalum wa kimahesabu kwa kushirikiana na kitengo cha Fedha ili kurahisisha shughuli zote na kifedha.· Bado kuna tatizo la kurudisha uthibitisho wa matumizi baada ya Hundi kutoka kama risiti, invoice na maelezo. 3.3 Mikakati 20101. Kuimarisha uongozi mzima wa kitengo hichi kwa kuhakikisha kila mwenye majukumu anayatekeleza.2. Kutokana na kupanuka kwa Jumuiya kwa kuongezeka shughuli zake, itabidi mfumo mzima wa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi utafutiwe utaratibu mpya wa kitaalam zaidi.3. Kutafuta wasaidizi wenye ujuzi wa masuala ya kimahesabu ili kuweza kutupatia misaada katika kuhifadhi kumbukumbu za mahesabu kitaalamu.4. Kuboresha ushirikiano na mawasiliano na vitengo vingine katika kupeana mahesabu ya matumizi na mapato. 4. Ripoti ya Kamati ya Da’awahMojawapo katika mipangilio ambayo Kamati ya Da’awah ilijaribu kufuatilia ni suala la kutuwezesha kuwa na kitengo cha Hajj ndani ya Jumuiya kitakachosimamia suala hili ikiwa ni kama mojawapo ya harakati zetu. Hata hivyo licha ya jitihada kufanyika katika kufuatilia kwa sehemu husika suala hili lilishindikana kwa sababu ya tayari kuwepo mawakala wa Hajj-Hajj Agency nyingi sana hapa Uingereza na Ubalozi wa Saudia kuzuia kuandikisha nyengine. Ubalozi umezuia kuandikisha Wakala nyengine kwa muda wa miaka mitatu.Kamati ya Da’awah ilihakikisha harakati za Da’awah zinaendelea katika mji wa Northampton na vitongoji vyake.4.1 Mafanikio· Kuweza kufanya Mihaadhara ya kila miezi mitatu ambapo kwa mara hii tulibahatika kumpata Ustaadh Badr Ja’afar kutoka nchini Kenya na kuweza kunufaika na Mada zilizotolewa.· Kuweza kusimamia Darsa la akinamama kwa kulipangia muundo wa usomeshwaji wa Walimu kupishana katika kuliendesha.· Kuweza kumsilimisha ndugu yetu mmoja na kuweza kumsaidia katika upande wa kimasomo kuweza kuifahamu dini yake.· Kuweza kuendesha programu ya Ramadhaan ambayo iliendeshwa katika njia ya darsa na kwa Ramadhaan ya mwaka 1430 programu ililenga zaidi kwenye Swalaah.· Kuweza kusali Sala ya Eidul Fitwr kwenye kiwanja cha KingsHeath. · Kuweza kukusanya Sadaqatul Fitwr na kuhakikisha inawafika walengwa kwa wakati wake muafaka.· Kuweza kuandaa Semina maalum kwa Wanashuraa iliyolenga katika kuwajenga kimanhaj na kiaqiydah na pia kutoa rasimu ya mfumo mzima wa Shuraa na jinsi itakavyoweza kutekelezwa kulingana na jumuiya yetu.· Kuweza kushirikana na ndugu zetu wa kisomali katika kuendesha na kusimamia Sala za Taraweih na Witr – SpringBorough. · Kuweza kuendeleza darsa la kinamama la mtandaoni - online ambalo linaendelea na kupanuka na lina wanafunzi zaidi ya 30 ikijumuisha Northampton, Ketering , Leicester na London.· Kuweza kuendeleza darsa la akinababa la Ustaadh Jaafar ambalo kwa sasa limehamia online kwa muda lina wanafunzi 9 wakiwemo wanashura wawili. · Kuweza kuendeleza darsa la akinababa la Ustaadh Baawazir ambalo kwa sasa lina wanafunzi 13 wakiwemo wanashuraa wawili. · Kwa ujumla kuna Wanashuraa wane tayari wanajiendeleza katika Madarsa yaliyotajwa. 3.2 Matatizo· Mahudhurio kwenye harakati nyingi za Jumuiya hasa zinazohusiana na Da’awah yamekuwa hayaridhishi. · Kutokusali Eidul Adh ha kwa pamoja ambapo ilibidi tuisali Misikitini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu. · Kudorora na hatimae kusita kwa darsa la akinamama kulikotokana na sababu ya mahudhurio kuwa hayaridhishi. · Kujitokeza kwa baadhi ya makundi ambayo yana lengo la kwenda kinyume na Al –Iman na kuendesha harakati zao kwa lengo la kudhoofisha malengo ya Jumuiya na pia kuleta mafundisho yanayokwenda kinyumne na malengo ya Al –Iman. · Kutofanyiwa kazi mafundisho yanayotolewa na hivyo kuathiri juhudi na nguvu zinazotumika katika kutafuta Wahaadhiri, kuandaa ukumbi pamoja na masuala mengine.3.3 Mikakati · Moja katika malengo makuu ya kamati ni kuiboresha Shuraa yetu kiitikadi, kielimu na kimanhaj na maadili ili iweze kwenda sambamba na sifa za uongozi, Manhaj pamoja Itikadi. · Kuandaa Semina mbili kwa uchache za uongozi pamoja semina ya akinamama · Kuandaa Mihaadhara kila baada ya miezi mitatu kwa Kiswahili na Kiiengereza. · Kuihuisha darsa ya akinamama. · Kujaribu mfumo mwengine wa kuziendesha darsa za Ramadhaan 5. Madrassah Madrasah iliendelea kusomesha watoto katika jengo la muda la Alliston Gardens kwa mwezi wa Januari. Mwishoni wa mwezi wa Januari Madrasah ilihamia kwenye jengo letu Cowper Street.Madrasah iliendelea hapo kwa muda wa mwezo mmoja na nusu hadi katikati ya mwezi March ambapo Madrasah ilisimamishwa ili kupisha hatua za upatikanaji wa kibali cha matumizi ya Jengo. Madrasah ilianzisha mfumo wa siku za wiki na siku za mwisho wa wiki Cowper Street ili kuweza kupata nafasi nyingi za kusomesha watoto.Kuyumba kwa Madrasah lilikuwa suala ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wanafunzi pamoja na na maendeleo ya Madrasah kwa ujumla. Suala hili lilikuwa nje ya uwezo wetu kwani tuliona jinsi tulivyopata taabu wakati tukitumia jengo la Alliston Gardens na tulipotarajia kwamba tumetulia pia tukapata misuko misuko mengine.Kwa ujumla licha ya Madrasah kufungwa baadhi ya walimu waliendeleza wanafunzi katika majumba yao ili kuwasaidia wasisahau masomo yao na pia wazazi pia waliwasaidia watoto wao majumbani. Hili tumeweza kulithibitisha kwani tulipoweza kufungua Madrasah tuliona baadhi ya watoto waliokuwa wakipata msaada hawakuathirika sana kimasomo tofauti na wale waliokuwa hawana msaada wa aina yoyote.Na kwa uwezo wake Subhaanah, Madrasah ilifunguliwa tena mwezi October 2009 Markaz Masjid Abington Avenue.Madrasah sasa ina wanafunzi takriban 200 na Walimu 18 miongoni mwao wamo waliojitolea kuja siku zote yaani Jumamosi na Jumapili na wengine wamejitolea siku moja kutokana na hali zao.Ilipofunguliwa Madrasah, lilikuja wazo kutoka kwa uongozi wa Msikiti kwamba tuangalie fikra ya kuziunganisha Madrasah hizi mbili na zote ziwe katika mfumo mmoja na jina moja na pia ziwe chini uongozi mmoja.Fikra hii ilifikishwa kwa Walimu kutoa maoni na pia imefikishwa katika kamati ya Shura.ambao wengi wao waliona suala hili kuwa ni gumu kutokana na misingi yetu na misingi ya Northampton Islamic Academy kuwa tofauti na pia kwa kutekeleza suala hili ni kuondokana na malengo yetu tuliyojiwekea ya kuwa na Madrasah iliyo chini ya usimamizi wa Jumuiya.4.1 Mafanikio· Kuweza kuirudisha Madrasah katika Msikiti na hivyo kwa kiasi fulani kuwa na uhakika wa kuendelea kwake.· Kuweza kuweka mfumo madhubuti wa utendaji kwa kuanzisha Baraza la Wazee, kuhakikisha Walimu wanatoa commitment zao na kuhakikisha kuwepo na chochote cha kuwashukuru kwa utendaji wao.· Kuboresha utendaji kwa kuweka Adiministrator ambae atakuwa na majukumu ya kusimamia masuala ya watoto yasiyohusiana na masomo.· Kuweza kuwaandikisha watoto wote walioomba usajili na kuhakikisha Walimu wamepatikana wa kuweza kuwasomesha. ( Hatuna waiting list tena kwa muhula huu)· Kuweza kuandaa kozi ya watoto kwa mwezi mmoja April ambapo watoto wenye umri kati ya miaka 10 na 16 walifundishwa mambo ya kimsingi katika dini yao kama Fiqh.’Aqiydah na Akhlaaq.· Kuweza kuwatenga watoto katika Darsa za Ramadhaan na kuwaandalia kozi yao maalum kwa lugha ya kiiengereza ambayo iliwasaidia sana kwani mara nyingi Masomo yanayotolewa Ramadhaan huwalenga wakubwa zaidi.· Kuandaa First aid Course kwa Walimu na wote kuweza kupata shahada.4.2 Matatizo· Bado Commitment ya baadhi ya Walimu ina matatizo na kutohudhuria kwa Walimu kuathiri maendeleo ya wanafunzi.· Kuyumba kwa Madrasah ambapo katika mwaka huu Madrasah ilianzia Alliston Gardens kisha kuhamia Cowper Street na baadae kufungwa kwa miezi minane kabla ya kufunguliwa tena kwa kurudi Msikitini pia huathiri maendeleo ya watoto kwa kutokuwa na utulivu katika masomo.· Malipo ya ada bado pia ni tatizo kwa baadhi ya Wazazi ambao licha ya kupewa barua za kukumbushwa bado hudiriki kuchelewesha ada· Licha ya kuanzishwa Baraza la Wazee lakini linaonekana bado halijaanza kuchukua majukumu yake ya kuisimamia Madrasah.· Bado Uongozi wa Marasah haujakamilisha taratibu muhimu za Walimu kama CRB .4.3 Mikakati 1431- 2010Madrasah katika moja ya kuboresha utendaji na maendeleo ya wanafunzi imejaribu kujipanga tena baada ya kufunguliwa na kuja na mikakati ifuatayo:· Kujaribu kuhakikisha ina Walimu wa kutosha kutokana na idadi ya wanafunzi. · Kuona umuhimu wa mchango wa Walimu na hivyo kuwepo angalau chochote cha kuwapa motisha kwa kazi wanayoitekeleza.· Kuunda nafasi ya Administrator ambaye atakuwa na hadhi kama ya Mwalimu atakaeshughulikia masuala ya kiutawala na hivyo kuwapunguzia mzigo Walimu ambao watajikita zaidi katika masuala ya ufundishwaji.· Kuhakikisha taratibu za kiusajili hasa kwa Walimu katika kufuatilia masuala ya CRB na child protection yanakamilishwa na Walimu wote ikiwa kama ni mojawapo ya taratibu za kisheria.· Kuandaa nidhamu nzuri ya Malipo kwa kuhakikisha malipo yanalipwa mwanzo wa mwezi badala ya mwisho wa mwezi na pia kufikiria njia ya kulipa kwa standing order kuepukana na usumbufu.· Kuhakikisha kila mzazi amepata nakala yake ya kujua taratibu za Madrasah – Madrasah guidelines. 6. KinamamaMiongoni mwa agenda muhimu zinazowahusu kina mama katika mwaka 1430 hijiria sawa na 2009 ni hizi zifuatazo: 6.1Darsa za kinamama na Walimu.Kwa mwaka huu 2009 darsa zetu za kila wiki pamoja na Walimu, tulikuwa na zoezi la wiki nne kwa kila Mwalimu. Hii ilileta hamu kubwa kwa wana darsa na kuweza kufuatilia kila somo kwa kina na kwa mtiririko mufaka.Faida: - Kufaidika na mfululizo wa mada moja kwa moja- Kumaliza mada nzima ya Tohara, pamoja na kugusia mambo mengi muhimu yanayowahusu kinamama miongoni mwa hedhi, nifasi, istihadha, ghusul na mengineyo.- Katika somo la aqiydah tulipata kufunuka zaidi juu ya manhaji ya sawa sawa pamoja na kuwa na hadhari ya makundi mbali mabli ya kidini yanayojitokeza hasa katika wakati huu tulionao.- Kupata fursa nzuri kina mama kuzungumza na kupanga mambo mengi yanayowahusu wao na jamii kwa ujumla. Kasoro - Kupatikana mahudhurio machache kwa kina mama, na wengi wao ni kutokana na sababu zisizoweza kuepukika kama vile ugonjwa, ujauzito, uzazi na mengineyo.- Kuvunjika moyo kwa walimu kutokana na mahudhurio pamoja na uchache wa wanafunzi wanaofuatilia masomo kikamilifu.- Baadhi ya kinamama kuwa wazito na kuchukua muda mrefu kurudi na kuendelea tena na darsa baada ya kutulia kutokana na sababu zilizokuwa zikiwakwamisha.- Kutopata fursa ya kumalizia mwalimu wa mwisho (Ustadh Jaafar) kama ilivyopangwa, katika masomo ya quraan pamoja kiarabu. - Kusita kwa darsa kwa kipindi kirefu tangu kabla ya Ramadhan hadi hivi sasa, ambayo hupelekea baadhi ya kinamama kutojishughulisha na harakati zozote za kidini. 6.2 Darsa la kwenye mtandao (Online Darsah) Online darsa ilianzishwa Mwezi wa Ramadhan 1429 Hijiria na kuendelea hadi vivi sasa. Alhamdulillah inaendelea vizuri hadi kupelekea kupanga mikakati muhimu ya kuboresha darsa hii baada ya kuona faida na matunda mazuri miongoni mwa wengi wanaozifuatilia. Baadhi ya mikakati hiyo ni; - Kuweka time-table maalum na kila mwana darsa kuijua na kuifuatilia- Kupanga makundi mbali mbali kutokana na ufahamu wa kinamama- Kuongezeka kwa walimu miongoni mwa kinamama ambao ni wanafunzi waliokuwepo siku nyingi na kupiga hatua nzuri, kuwa na wanafunzi wao huku na wao wenyewe kujiendeleza.- Kuweka kumbukumbu za wanafunzi wote waliojiunga pamoja na repoti ya maendeleo yao. - Masomo tunayoendelea nayo ni; Kusoma Quraan, Elimu ya Tajweed na HadithWanafunzi zaidi ya 33 walijiunga, kati ya hao ni 22 tu wanaendelea na Darsa. Na kati ya wanafunzi wote kwa ujumla ni 14 tu ndio wakazi wa Northamptonshire na waliobaki wanatokea London, Leicester na Reading. Faida: - Kina mama wengi wanajitahidi kutenga muda wao kwa ajili ya darsa licha ya kutigwa na mambo mengi ya kijamii na kifamilia.- Kuwa ni fursa nzuri kwa wale wasioweza kuhudhuria darsa za ana kwa ana kutokana na sababu za kiafya, uja uzito, ulezi, umbali, usafiri na mengineyo.- Kuwa na mapenzi ya kusoma na kufuatilia quraan kwa kina, pamoja na kutenga muda wa ziada mbali ya ule wa online.- Wanafunzi wengi kupata tashjii (moyo) na kujizowesha kusoma wenyewe (self-studies) masomo ya dini pamoja na kupata fursa nzuri ya kuchangia wakati masomo. - Walimu kinamama hupata fursa muafaka ya kujiendeleza kwa kina pamoja na ustadh juu ya elimu ya quraan pamoja na lugha.Kasoro: - Kidogo huwapa uzito wanafunzi beginner kwa kukosa mwalimu wa ana kwa ana.- Baadhi ya kina mama huwa wasahaulifu haraka wa sura za nyuma.- Kuwakosa wengi miongoni mwa wale walengwa wa mwanzo (wanadarsa wa Northampton) na kujikuta wageni ni wengi wa miji mbali mbali wanaofuatilia na kupiga hatua nzuri kimasomo.- Uchache wa walimu wa kudumu 6.3 Ramadhaan 1430Alhamdulillah shughuli za Ramadhaan kwa upande wa kina mama zilikwenda kama zilivyopangwa. Baadhi ya harakati tulizozifanya ni pamoja na:- Kupata fursa ya kusikilizana quraan kwenye holi ana kwa ana.- Wanafunzi wa kike wakubwa pamoja na wageni wasiozungumza Kiswahili kutengewa muda wa darsa kwa kiingereza.- Kupata wadhamini wa kutosha katika maandalizi ya darsa pamoja na futari.- Kuendeleza darsa za online kwa kipindi kizima cha ramadhan6.4. Shughuli za EidAlhamdulillah shughuli zote za eid zilikwenda kama zilivyopangwa, tumeweza kutunisha mfuko katika shughuli za kina mama na watoto katika program zilizoandaliwa Berzerk na Northampton Academy.. 6.5 Agenda ndogo ndogo:Msiba: Katika mwaka huu tulipata taarifa za kushughulikia fardhi (maiti) kwa kina mama mara mbili. Moja (Msomali) kwa kupitia moja kwa moja Al-iman, kupewa taarifa rasmi, na kufanya shughuli zote za uoshaji na kukafini. Nyengine ni (Mkenya) kutoka Milton Keyns, mama mfiwa alikuja Northampton na kutaka msaada wa kushughulikiwa maiti yake (mtoto wa kike) na wanadarsa wa hapa.Mapendekezo: Ni vyema kuwe na mfumo maalum wa kushughulikia jambo hili isiwe inafanywa kiholela, na wafiwa kuchangia chochote kwa wale wanaoshughulika pindi ikiwa hayupo katika mfuko wa msiba. Mialiko: Moja kati ya harakati za kina mama ni kujishughulisha na mialiko mema katika jamii. Alhamdulillah tunapatapa mialiko mingi ya arusi na kujitahidi kushikirikiana na wahusika kikamilifu katika kuondoa yasiofaa. Wengi wao wanakubali masharti tunayowapa; kama vile kusiwe na aina yeyote ya recording, kuepuka michanganyiko ya kiume na kike na mengineyo. Kasoro za hapa na pale haziwachi kujitokeza.6.6 Uongozi wa akinamama.Tunashukuru miongoni mwa wengi wa kinamama walioteuliwa na kupeana majukumu wanajitahidi kuyafanyia kazi majukumu yao. Umoja na ushirikiano upo wa hali ya juu hasa likitokea lolote linalowahusu kina mama huwa ni kitu kimoja.7. Mfuko wa Misiba 1429/30 - 2009Mfuko wa Misiba ni mchango ulioanzishwa na jumuiya ya Al-iman ya Northamptonshire ili kusaidia gharama za mazishi kwa watakao fariki au kufiwa na jamaa zao ambao wanaishi nao na kuwahudumia. Hii ni kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kujigharamia wao wenyewe ikiwa kwa ujumla au baadhi ya gharama hizo.Mfuko huu umeshatimiza miaka 5 tokea kuanzishwa kwake hapo mwaka 2004. Mfuko huu wa Misiba unajumuisha kamati ndogo ndogo kutoka upande wa akina mama na akina baba na zote zinafanya kazi sambamba na kwa mashirikiano kutokana na taratibu ambazo tumejiwekea katika kufanikisha yale ambayo tunayakusudia.Kamati hizi zote zina viongozi wake ambao wamechaguwana na kujipangia taratibu zao.7.1 KamatiØ Kamati ya ufuatiliaji na upatikanaji mwili wa marehemuØ Kamati ya uoshaji na ukafiniØ Kamati ya DaawahØ Kamati ya kuhudumia wafiwaØ Kamati ya kuongoza mkusanyikoØ Kamati ya vifaa vya kuzikiaØ Kamati ya kukusanyaji michango 7.2 Utendaji:Kwa bahati mbaya utendaji katika kuendesha Mfuko huu sio wa kuridhisha sana kutokana na baadhi ya watendaji kukosa ari au kukosa muda wa kushughulikia dhamana zao ambazo wako nazo.Huko nyuma mfuko uliunda majimbo na kuteuwa wawakilishi wa majimbo yenyewe ili kurahisisha mawasiliano baina ya wachangiaji na uongozi na pia ukusanyaji wa michango lakini kwa bahati mbaya wawakilishi wengi wamesiahau. Hii inatokana aidha kusahau wajibu wao au kuchoshwa na walengwa wenyewe ambao huwa hawathamini juhudi zinazochukuliwa.Hata hivyo katika hali hii hii ya kuchechemea bado tuna kila hali ya kujivunia hapa tulipofikia. Katika mbinu yakuboresha utendaji tumejaribu kuongeza nguvu kwa kumshawishi ustaadh Shani kuwa mshauri wetu. Katika mwaka huu tuliweza kufanya vikao vya mara kwa mara na hasa pale panapotokezea tukio,vile vile tuliweza kuwaita wachangiaji wa mfuko huu kutoka jimbo la Milton Kynes kwa madhumuni ya kujuwana na kuwapa muongozo na kuwashuri kuchaguwa uongozi wao na kujipanga vyema iwapo patatokezea fardhi miongoni mwao. Mfuko ulikuwa umefikiria kuwaachia majukumu wenyewe ifikapo January 2010 lakini imeonekana haitowezekana kutokana na haya matatizo yaliopo. Tarehe 13/12/09 tulipata mualiko kutoka Milton Keynes katika harakati za kuboresha mambo ya mazishi na tulikubaliana kufunguwa ukurasa mpya na kuweka malengo ya muda mfupi na kukubaliana kukutana tena baada ya miezi 3 ili kutathmini yale yaloyeza kutendeka.7.3 Mafanikio:· Katika kujitahidi kwetu tumefanikiwa kupata ruhusa ya kuzika bila ya kupitia kwa Mkurugenzi wa mazishi kuotoka nje, vile vile kuzika bila ya kutumia sanduku na pia kupata kaburi ambalo tumelizowea lenye mwanandani. · Kutokana hatua hii Jumuiya imo mbioni kuandaa Idara nyengine ambayo itashughulia masuala haya kwa kushirikiana na mfuko wa misiba· Kwa upande wa uchangiaji, wameongezeka ki idadi (wapya) lakini michango imepunguwa,Kutokana na hali hii mfuko uliamua kuondowa adhabu ya kumfuta mchangiaji alie na malimbikizo ya muda mrefu na badala yake kutowa nafasi ya kuchangia kwa kulipa malimbikizo yake.Vile vile wale wachangiaji ambao walijiorodhesha tu na kukaa muda mrefu bila ya kuanza kuchangia waliwashauriwa kuanza upya na kutokana na zoezi hili mfuko umeweza kukusanya kiwango kikubwa cha malimbikizo. 7.4 Matukio: Mwaka huu tulipata fardhi 3 1. Tarehe 13/03/09 mtoto wa kiume ambae hakuwa mchangiaji (Malipo ya huduma yalitolewa) 2. Tarehe 01/07/09 Stillborn mchangiaji alie na malimbikizo. (Alisaidiwa) 3. Tarehe 23/10/09 mtumzima mwanamke, hakuwa mchangiaji.(Malipo ya huduma yalitolewa) 7.5 Matatizo:· Kitengo bado kinakabiliwa na tatizo lile lile latokea mwaka ulopita la viongozi wake kutokuwa na ari ya utendaji na kutekeleza majukumu ambayo waliyachukuwa. Kwa ridhaa zao.kutokea kwenya ngazi ya ari ya uendji · Uchangiaji bado linabaki kuwa ni tatizo sugu, hii inatokana na uzito wa wachangiaji na taratibu zetu bado si madhubuti, hivyo wengi wa waumini wanatumia nafasi hii kutotimiza majukumu yao. Ili kukabiliana na tatizo hili tunategemea kulipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kila ataependa kubakia kuwa mchangiaji wa mfuko huu. · Wachangiaji kushindwa kutowa taarifa pale panapotokezea mabadiliko katika nyumba zao kama vile kuongezeka kwa familia,kuhama,kubadilika kwa jina na kadhalika, · Jimbo la Milton Keynes bado linabaki kuwa ni mzigo mkubwa kwetu kutokana na kukosekana kwa umoja na mashirikiano katika mji huo kwani watu wamejigawa makundi makundi.Mbali ya kuwa tulikutana na wachangiaji na kupeana majukumu lakini bado kuna ugumu katika utendaji,huenda mkutano wete wa 13/12/09 ukazaa matunda. · Jimbo la Wellingborough haliko imara katika uchangiaji ingawa muwakilishi wake yuko na bidii ya kuufikisha ujumbe pamoja na ufatiliaji. · Utaratibu wa kuwaelimisha waumini umuhimu wa mfuko bado si mzuri, kwani mpaka patokee fardhi ndio utaona waumini wanajitokeza kuchukua fomu, hii inaonyesha kitengo cha misiba bado kina kazi ya kuwaelimisha waumini umuhimu wa mfuko na lengo lake, na si kusubiri fardhi ndio iwape ujumbe huo. 7.6 Mapato: 1, Malimbikizo ya mwaka 2007 kuja 2009………………………£50.00 kati ya £850.00 2. Malimbikizo ya mwaka 2008 kuja 2009…………………£1,230.00 kati ya £4,495.00 3. Mchango wa mwaka 2009 zilizilipwa mapema 2008… £180.00 (zimeingia katika hesabu ya Mwaka 2008) 4. Michango ya mwaka 2009 ………………………………………£4.815.00 5. Mchango wa mwaka 2010 zilizolipwa mapema 2009…….. £355.00 6. Michango ya huduma………………………………………. £239.34 Jumla ya makusanyo ya mwaka 2009 £ 6689.34 Mpaka kufikia 30/12/2009 Mfuko wa misiba una jumla £ 27,256.84 7.7 Matumizi 22/01/09 Vifaa vya ofisi…………………………….. ………………….. £560.0026/06/09 Gharama za usafiri kushgulikia sanduku la kubebea maiti £ 59.4424/10/09 Adaya ya kuwekewa tangazo katika kitabu NHS £395.0008/11/09 Ununuzi wa sanduku la kubebea maiti £95.0008/10/09 Gharama za usafiri kuchukuwa sanduku £30.00 Jumla £ 1,139.44 7.8 Malengo ya Mwaka 2010 · Ili kurahisisha ukusanyaji wa michango, wachangiaji wote watalazimika kulipia michango yao kupitia bank kwa njia ya Standing Order au Direct Debit zoezi ambalo tunategemea kulikamilisha haraka iwezekanavyo Insha allah. Barua za kuelezea maamuzi haya Kwa zilishaanza kusambazwa kwa wachangiaji na bado zinaendelea. Mchangiaji yeyote ambae hatoweza kufata utaratibu huu itamlazimu awasilianae na uongozi iwapo bado anataka kuendelea kuwa mchangiaji. · Ungozi umekubaliana kutowa ubani wa £200.00 iwapo patatokezea fardhi kwa mchangiaji ambae ana familiya yake huko alikotoka. Atakae weza kufaidika na ubani huu ni yule mchangiaji ambae hana malimbikizo yoyote na kabla ya kutowa ubani huu tutafanya uchunguzi wa kina wa kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa ni sahihi ili kuepusha udanganyifu. · Waliokubalika kutolewa ubani huu ni hawa: o Baba mzazio Mama mzazio Mtoto wa kumzaa · Kuwa na usafiri wa uhakika kwa matumizi ya Mazishi na wakati huo huo usafiri utaoweza kutumika katika shughuli nyengine yenye kuweza kuzalisha na kukubalika kisheria · Kuufanyia marekibisho muundo wa mfuko wa misiba ili uendane na mabadiliko yaliyotokea. · Kufanya angalizo kwa wawakilishi na wakusanyaji ili kuhakikisha wanajua malengo yao na kuweka utaratibu maalum wa kufuatilia · Kuhakikisha uongozi wa juu wa Mfuko wanayafahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo. · Kuliimarisha jimbo la Wellingborough ingawaje muwakilishi wa huko yuko imara lakini walengwa wenye ndio matatizo. v Tutaendelea bila ya kuchoka kuutangaza mfuko ingawaje jamii yetu inafahamu vyema faida faida zake. v Kuwa na mawasiliano mazuri na kitengo cha akina mama kwa kuwapa taarifa kila panapotokezea mabadiliko. 7.8 Pendekezo: Kitengo cha Misiba kinapendekeza kubadili jina la mfuko badala ya kuwa Mfuko wa Misiba liwe Mfuko wa Huduma ya mazishi / Funeral Support Fund ili liweze kwenda sambamba na malengo yake. 8. Fund Raising 8.1 UtanguliziKitengo hichi kilianzishwa mwanzoni mwa mwaka huu 2009, baada ya kuona kuwa Jumuiya ya Al-Iman inahitaji kitengo hichi kutokana na hatua tuliofikia na mahitaji ya Jumuiya kwa kipindi hichi, ambapo Jumuiya imefikia hatua kubwa Al-hamdullilah na inahitaji zaidi rasilimali za hali na mali ili kuipeleka mbele. Kazi kubwa ya kitengo hichi ni kuisaidia kutunisha mfuko wa Jumuiya. 8.2 Njia za kutunisha mfuko; · Kutuma proposal kwa Jumuiya za kitaifa na za kimataifa (Potential Donors Organisation) na watu binafsi, kwa ajili ya kuomba misaada kwa maendeleo ya Jumuiya, hasa utafutaji jingo, itakuwa inayokubaliana na katiba ya Jumuiya.· Kuandaa Tamasha mbalimbali na matukio mengine ya kiislamu ili kutunisha mfuko kwa njia ya kujitolea, kama sadaka, kiingilio, minada, kuuza vyakula na bidhaa nyingine n.k· Kugawa maeneo nadharia (Hypothetical Square Metre), ambayo yatapigiwa hesabu kutokana na maeneo halisi au eneo linalotegemewa kukidhi ukubwa unaotegemewa wa ujenzi au ununuzi wa jingo la Jumuiya. Kila muumini ambaye atachangia au atataka kununua eneo lake atawajibika kulipia kiwango cha fedha (Token Fee) kwa muda ambao utapigiwa mahesabu kukidhi muda halisi wa ujenzi au ununuzi wa eneo (Actual Milestone)· Kutafuta namna ya kuanzisha mradi ambao utapelekea kuzalisha kwa faida ili kupunguza hali ya Jumuiya kuwa tegemezi kwa siku za baadae. Hili linawezekana kwa kuchukua mifano ya Jumuiya nyingine zenye malengo na mwenendo kama wetu.· Kutengeneza visanduku maalum vya kuchangisha michango kutoka kwa waumini mbalimbali na kuviweka katika sehemu mbalimbali.· Kuandika barua kwa baadhi ya misikiti hapo Uingereza kuweza kufanya michango katika misikiti hiyo 8.3 Mapendekezo · Kuandaa vipeperushi vyenye mvuto na maelezo yenye kueleweka zitakazo onyesha Jumuiya yenye na malengo yake kwa ufupi.· Kuandaa Muhtasar wa Jumuiya (Organization Profile) ili kuitambulisha Jumuiya yetu na malengo yetu kwa urefu. Muhtasar huu utatumika kama kiambatanisho pindi tutakapo tuma maombi yetu popote misaada au kujitambulisha.· Kuandaa mahesabu halisi ya eneo la ujunje au kununua· Kuandaa bajeti halisi na bajeti nadhariana na vielelezo vya bajeti.· Kuandaa maelezo maalum (Information pack) ambayo yataandaliwa katika hali nzuri, yenye nembo anuani na vielelezo vyo vya Jumuiya ya Al-Iman. Maelezo haya yatakuwa yanajumuisha, barua ya utambulisho, vipeperushi, Muhtasar wa Jumuiya, mafanikio ya Jumuiya na mengineyo yote yanayohusu Jumuiya yetu. · Kuanzisha jarida la Jumuiya ambalo litakuwa linatumwa kwa waumini. Jarida hilo latahusisha masuala yote ya Jumuiya kwa ujumla na habari nyingine za kiislamu. 8.4 Mafanikio· Kamati imefanikiwa kuandaa Muhtasari wa Jumuiya (Organization Profile), ambayo ndio inatumika mpaka sasa hivi.· Kamati imeweza kusambaza visanduku vidovidogo sehemu mbalimbali kwa ajili ya sadaka za waumini.· Kitengo cha Fund Raising kikishirikiana na kamati ya vijana na michezo kimefanikiwa kufanya ghafla mbalimbali kwa ajili ya kutunisha mfuko wa Jumuiya.· Kuandika barua maalum kwa karibu misikiti mingi hapa Uingereza kwa ajili ya kujitambulisha na kuomba misaada.· Tumefanikiwa kuwa na vipeperushi vyetu maalum vya kuitambulisha Jumuiya na harakati zake na kuvisambaza sehemu mbalimbali.· Kukusanya michango kwa karibu misikiti miwili mmojawapo ukiwa hapa hapa Northampton. 8.5 Matatizo § Mpaka sasa hivi kitengo hiki cha hakijapata mfumo wake na muundo maalum unaoelezea wazi uendeshwaji wa kitengo hichi.§ Timu bado inahitaji wasaidizi wenye ujuzi na kujituma.§ Pamoja na kwamba tumefanikiwa kuandika barua kwa zaidi ya misikiti isiyopungua 100 mpaka sasa hivi hatujafanikiwa kupata majibu yoyote kutoka kwa misikiti hiyo, isipokuwa mmoja tu London.§ Zoezi la kutuma na kuandaa vipeperushi limesita kutokana na upungufu wa fedha, ambapo gharama za uchapishaji na utumaji zimekuwa kubwa.§ Matukio na ghafla karibu zote hazikuweza kutunisha mfuko kiasi kikubwa kwa sababu lengo linakuwa zaidi kuhudumia waumini na si zaidi kutunisha mfuko.§ Hakuna jarida lililoanzishwa.§ Kifurushi cha maelezo (Information Pack) hakikukamilika kutokana kukosekana baadhi ya vielelezo. 8.6 Mikakati 2010· Kuandaa muongozo maalum wa kitengo (Katiba)· Kuunda timu madhubuti · Kupunguza baadhi ya malengo na kuyapitia mengine ili kuwa halisi zaidi na si kujichanganya na kuweka malengo yalio nje ya uwezo wetu.· Kuwa na ratiba maalum ya kuendesha shughuli za kitengo· Kuweka maelezo na mahesabu kitaalam zaidi. 9 Uratibuti wa Shughuli za Jumuiya. 9.1 Matukio ya Jumuiya Katika Kipindi Cha Mwezi Ramadhaan Na Eid Ul Fitr 1430 (2009).Maandalizi ya mwezi mtukufu wa Ramadhaan yalianza kwa kikao cha shuura ambapo wanashuura walikuwa katika hali ngumu, juu ya kutoa maamuzi kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa darsa za Ramadhan kwa mwaka huu wa 2009 (1430). Katika kikao hicho wana shuura walikubaliana kuwepo kwa darsa baada ya kujitokeza wadhamini walioweza kujitolea kwa kiasi fulani kufanikisha baadhi ya gharama muhimu za kuanzia.Darsa za mwezi mtukufu wa Ramadhaan zilianza kwa mhadhara maalum wa kuukaribisha mwezi mtukufu, ambapo mhadhiri wake kwa kawaida ni sheikh Feisal kutoka Leicester.Katika mwezi mtukufu mada kadhaa ziliwakilishwa na kupatikana faida kubwa kwa wana Jumuiya,japo kuwa mahudhurio hayakuwa mazuri lakini darsa zimeleta faida kwa wale wachache waliohudhuria. Ili kufanikisha Darsa hii muhimu, kamati ya Shu’ra ili amua kianzishwe kitengo maalum cha Coordinator , ambacho kitasaidia kuandaa na kusimamia shughuli zote za Jumuiya, si kwa kipindi cha Darsa za Ramadhaan tu, hata kwa shughuli nyingine za Jumuiya za kila siku. Na ilikuwa wakati muafaka kwa sababu, Mwezi mtukufu wa Ramadhaan ulikuwa inakaribia, ikaonekana itakuwa ni fursa nzuri kwa kitengo hiki kipya kuanza kazi zake, zifuatazo kwa ufupi ni kazi za Mratibu;· Mawasiliano na wakuu wa vitengo· Ripoti· Kuhakikisha wakuu wa vitengo wanasimamia vitengo vyao· Kuangalia upungufu wowote wa maandalizi ya shughuli.· Kutatua matatizo yatakayo jitokeza wakati wa hughuli· Kufanya tathmini ya matukio/shughuli za Jumuiya Kitengo hiki bado ni kichanga sana na kinaendelea kujifunza katika kuhakikisha shughuli za Jumuiya zinafanyika kiutaratibu. Darsa za mfungo huu uliopita wa mwezi mtukufu wa Ramadhaan ni uzoefu pekee uliopatikana kwa kitengo hichi. Pamoja na kwamba hakukuwa na tofauti kubwa na Darsa zilizopita lakini tumejifunza mengi ambayo yatatusaidia katika shughuli zetu za kila siku. Jumuiya ya Al-Iman ina vitengo vidogo vidogo vya kushughulikia uendeshaji wa shughuli zote za Jumuiya, lakini kulikuwa hakuna mratibu maalum wa kuhakikisha vitengo hivi vinafanya kazi zake ipasavyo, na uzoefu umeonyesha hiki ni kitengo muhimu sana kama kitafanya kazi kama inavyotakiwa. Nguvu za Jumuiya ziko katika kubuni matukio na inaonekana kuwa Jumuiya inao watu wenye uwezo wa kubuni matukio na kuipeleka Jumuiya mbele.Lakini Jumuiya ina udhaifu katika utendaji na usimamizi wa matukio, na hili lipo wazi kabisa kama ilivyo dhihiri katika idara mbali mbali. Idara nyingi bado hazina wawakilishi wa kutosha na kudumu kutekeleza majukumu yao. Tatizo hili linapelekea baadhi wa wahudumu kuwa na kazi za ziada kwa sababu hawana wasaidizi au baadhi yao hawatekelezi majukumu yao.Kuna matatizo makubwa katika vitendea kazi (resources), ki fedha kama inavyofahamika na pia kwa watendaji (manpower) Hakuna watendaji wa kutosha na pia hawa wachache waliopo ni 1/3 yao ndio waliojikubalisha (committed) hali hii inarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa.Moja ya sababu kubwa ya udhaifu wa Jumuiya yetu ni kuwa viongozi na wajumbe wa kamati ya Shura ndio hao hao watendaji wakuu wa Jumuiya, na wasimamizi wakuu wa shughuli na matukio yote ya Jumuiya, pamoja na kuwa kuna vitengo maalum vya usimamizi wa shughuli zetu, lakini tunarudi pale pale kuwa watu wenyewe ndio hao hao, na wengine wanakuwa na zaidi ya kitengo kimoja au zaidi vya kusimamia. Hii inasababisha kutokuwepo uangalizi na usimamizi wa uhakika, kwa sababu watenda kazi hawawezi kujiangalia wenyewe kwa sababu wao ndio viongozi.Wapo baadhi ya waumini ambao wako mstari wa mbele katika kujitolea kusimamia shughuli za Jumuiya lakini ni wachache sana kulinganisha na mahitaji ya shughuli za Jumuiya. Na tatizo hili haliishii kwenye matukio na shughuli za Jumuiya tu, bali hata katika idara nyingine za Jumuiya kama Madrassa na Kitengo cha Misiba, mfano Waalimu ndio hao hao Administrators na viongozi wa Misiba ndio hao hao wakusanyaji michango. Hii inaonyesha kuwa bado Jumuiya ya Al-Iman ina kazi kubwa ya kuwavuta waumini wa Northamptonshire si kuhudhuria tu mihadhara na Darsa bali pia kujihusisha na shughuli nyingine za Jumuiya yao mara kwa mara.Tatizo jingine ni kuwa pamoja na kuwa kila kitengo kina utaratibu wake wa kufanya shughuli zake, taratibu hizi lau hazifuatwi, zimepitwa na wakati au hazipo kabisa na nyingine zinabidi ziandikwe upya kabisa. Hili litasaidia kupata muelekeo wa kila kitengo ni jinsi gani au ni taratibu gani za kufuatwa katika kuendesha vitengo vyao. 9.2 MafanikioKuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika shughuli zetu za mwaka huu katika upande wa daawa na kijamii. Mafunzo yaliyotolewa kwa mfano katika sala na tunawanukuu baadhi ya waliohudhuria kukiri kuwa baadhi ya mafunzo yaliyotolewa ni mara yao ya kwanza kujifunza utaratibu huo ulofundishwa siku hiyo. Ni dhahir kwamba kuna wengi ambao hawakuweza kutamka lakini walikuwa katika hali kama hiyo, hali kadhalika tumeshuhudia watu wengi kujifunza nguzo za sala na wajibu wa sala na mada kuu iliyofundishwa ya sijida ya kusahau. Kijamii tunawashukuru wale wote waliofanikiwa katika kujitolea kwa hali na mali kufuturisha katika mwezi wa Ramadhaan Allah Subhaanahu wataalah anajua ujira wao sisi tunawaombea ujira huo uthibiti, na wasiishie hapo waendelee na moyo huo mpaka kufikia Ramadhaan nyingine.9.3 Matayarisho Ya Sherehe Za Eid ul FitirMatayarisho ya sherehe za Eid yalianzia kwa maandalizi ya sala ya Eid, ambapo kila kitu kilikwenda vizuri. Tunamshukuru Allah Subhaanahu wa taalah kwa kuwawezesha wahusika kufanikisha kwa uwezo wake.Baada ya sala kulikuwa na sherehe za Eid, jioni ya siku hiyo ya eid ambazo kwa mwaka huu ilikusudiwa kuwajumuisha watoto na wazee wao wa kike na wa kiume, kinyume na taratibu za kawaida za Jumuiya, ambapo washiriki huwa ni watoto na mama zao tu.Matayarisho yalikwenda vizuri pamoja na ukweli kuwa matatizo ya hapa na pale hayakukosekana.Utendaji ulikuwa kwa mfumo wa kugawana majukumu kwa watendaji mbalimbali, hivyo kazi ziliainishwa na kugaiwa kama ifuatavyo;1-Watayarishaji2-Wasimamizi9.4 ShukuraniUongozi wa Jumuiya unapenda kuwashukuru wanaJumuiya wote walioshiriki katika kufanikisha shughuli zote za Jumuiya kwa mwaka huu, Allah Subhaanahu wataala atawalipa ujira mkubwa. Kwa mwaka unaofuata ni vyema kwa uongozi wa Jumuiya kuziangalia gharama hizi na kuanza kuzifanyia kazi mapema. Vile vile kufanya marekebisho yanayohitajika ili kuweza kufanikisha shughuli hizi kwa kiwango cha juu. Kwa vile Jumuiya kama hizi za khiari ‘charity’ huwa zina fanyiwa tathmini kutokana na harakati -‘program’ inazoziendesha kwa mwaka ni vizuri kutilia mkazo utekelezaji wake kwani mafanikio ya program hizo ndio mafanikio ya Jumuiya. 10 Tovuti – WebsiteTimu ya wasimamizi wa tovuti iliendelea kuiendesha tovuti kwa malengo ya kurahisisha mawasiliano, kutumika kama ni sehemu ya elimu na hviyo kupata mafundisho kutokana na mada, makala, mawaidha pamoja na kuhifadhi kumbukumbu za Jumuiya ambazo zinakuwa rahisi kupatikana zikiwepo kwenye tovuti.Tovuti pia iliweka sehemu ya ukumbi – forum ambapo mawasiliano kati ya Wanajumuiya na Jumuiya yanapoweza kupatikana kwa kuweza kuleta maoni, mawazo na hata kuwekwa mambo yatakayoweza kuifaidisha jamii na kufundisha.Kuna sehemu maalum ya Kiingereza ambayo ina malengo la kuwafikishia habari hasa wasiozungumza lugha ya Kiswahili kuweza kupata taarifa, habari na matukio katika Jumuiya ya Al -Iman. Sehemu hii pia inalenga katika kuwasaidia wanafunzi wetu ambao tunatarajia watakuwa watumizi wakubwa katika kupata habari na hata ikiwezekana kutumika katika kusomeshea.Kwa upande wa makala zinazowekwa, kamati ya Da’awah imechukua jukumu la kuzihakiki, kuzipitia na kuzihariri ili ziendane na mfumo wa manhaj ya Jumuiya. 10.1 Mafanikio· Tovuti imeweza kuendelea kutuwekea habari, taarifa, makala na mawaidha· Kiungo cha mapishi ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kimedorora, kimehuika tena kwa kuweza kupata mmoja wa wanajumuiya aliyejitolea kutuletea mapishi.· Kuweza kuongeza kiungo cha Hadithi za Wiki ambacho pia kinasimamiwa na mmoja wa Wanashuraa ambaye amejitolea, atakapojaaliwa, kutuletea hadithi pamoja na maelezo yake.· Ukumbi uliweza kuhuishwa tena wa Wanashuraa kwa kuweka somo la tohara na pia kupata wachangiaji miongoni mwa wanajumuiya waliobahatika kusoma na kuuliza masuali.· Kuongezeka uwiano wa wanaotembelea tovuti ambapo kumeongezeka mara mbili ya waliokuwa wakitembelea kabla.· Kuweza kukamilisha kitabu cha Hadithi arubaini za Imaam Annawawiy ambazo zilikuwa zikiwekwa kila wiki hadithi moja moja. 10.2 Matatizo· Suala la usimamizi wa tovuti bado ni tatizo kwa sababu iliyoelezewa katika kipengele No 9 kwamba ni aina ya watu wale wale wanaoisimamia majukumu na hivyo kuwepo uzito katika utendaji.· Kuna viungo kama cha Video ambacho hakina kitu kilichowekwa tokea kuwepo kwake· Taarifa na habari kutoweza kuwekwa kila mara au zinapotokea – update10.3 MikakatiTimu inayosimamia, itajaribu kuboresha hali ya tovuti ili iendane na kasi ya maendeleo ya teknolojia kwa kurekebisha na kuongeza wasimamizi ikiwezekana.11 JengoMoja katika mikakati ya muda mrefu ya Jumuiya ni kuwa na jengo letu wenyewe litakalotuwezesha kuendesha shughuli na harakati zetu kwa ujumla. Katika mwaka 2008 jitihada hizi zilionesha mwelekeo tulipofanikiwa kulipata jengo liliopo 74-76 Cowper street na baada ya kushauriana yakapita maamuzi tulichukue kwa kulikodi.Jengo hili lilikuwa katika hali mbaya kwani lilikuwa likitumika zamani kama kiwanda cha kutengenezea viatu na hivyo likahitajia ukarabati mkubwa ambao uliweza kufanyika kuanzia mwishoni wa mwaka 2008 na kuendela katika mwaka 2009.Baada ya kumalizika ukarabati wa kwanza ndipo yalipofanyika maamuzi ya kuanza kutumika na kuanzia Januari 2009, Madrasah ilihamia katika jengo letu. Hata hivyo katika mwezi wa March 2009 tulipata barua kutoka Borough Council inayotutaka kusimamisha shughuli zetu kwenye jengo kwani kibali cha matumizi kilikuwa hakijombwa kutoka sehemu husika – planning permission.Kwa dharura iliyojitokeza ilitubidi tusimamishe shughuli zetu ili kufuatilia kibali kwani kabla tulishauriwa kwamba tunaweza kulitumia huku taratibu za maombi ya kibali zikiendelea.Tuliwasilisha maombi yetu Planning Commission tarehe 23/03/2009 hata hivyo yakawa yamekataliwa katika kikao kilichokaa tarehe 26/05/09.Sababu zilizotajwa na wanakamati wa WNDC Planning Commission katika kuyakataa maombi yetu ni kwamba sehemu jengo lilipo halina nafasi ya kuegesha magari na hivyo kuwaongezea mzigo wakaazi wa eneo na ya pili ni kuwepo kwa watoto katika sehemu ya jengo kunaweza kuleta zogo na kelele .Na kwa sababu hizi mbili kamati ilipiga kura na kura tatu zilikataa maombi yetu na kura moja tu ndiyo iliyoyakubali. Tumepewa muda wa miezi sita, kama hatujaridhika na maamuzi, kukata rufaaMaamuzi haya hayakuturidhisha na baada ya kikao cha Shuraa kilichokaa kiliona ni bora tukate Rufaa. Ingawa kulikuwa na wazo wa kuyapeleka maombi yetu tena kwa kubadilisha baadhi ya vipengele jambo ambalo hatukuona kama litaweza kutusaidia kwani timu itakayoshughulikia ingelikuwa ni ile ile iliyokataa maombi yetu ya awali.Rufaa iliwasilishwa katika mwezi wa Novemba 2009 na bado tupo katika kusubiri matokeo ya Rufaa hii ambayo tuliahidiwa itakuwa kati ya mwezi wa tatu au wanne 2010. 12 Hitimisho.Kama ripoti ilivyojionesha, hayo ndiyo mambo ambayo Jumuiya iliweza kufanikiwa kuyasimamia kwa mwaka 1429 - 2009.Jumuiya kwa ujumla inatanguliza shukrani za dhati kwanza kwa wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha harakati na kuweza kuifikisha Jumuiya katika hali iliyopo ambayo tunaweza kudiriki kusema ni kwa sababu ya Wanajumuiya kuona umuhimu wa kufanya harakati kwa ajili ya kuitengeneza Jamii pamoja na kuendeleza dini yetu ya kiislamu. Jumuiya ilipita katika kipindi kigumu katika mwaka huu tokea kuanzishwa hasa kutokana na kukwama harakati zake kwa kukosekana jengo ambalo bado tunaliendelea mbio tukiwa katika hatua ya Rufaa ha gharama nyingi za hali na mali katika kulifanyia ukarabati.Jumuiya imeona ipo haja ya kujipanga upya katika uongozi na utendaji na hivyo kuandaliwa mfumo mpya wa Shuraa ambao utawalenga viongozi wakuu wa Jumuiya ikiwa ni kama dira na mwelekeo utakaotuwezesha tuwe katika hali moja kimwelekeo, kimawazo na kimtazamo na hivyo kutuwezesha kuziendesha harakati katika misingi inayotakiwa kwa mujibu wa katiba yetu.Jumuiya ina mambo mengi inataka kuyatekeleza ila jambo linalotukwaza ni kwamba shughuli hizi huendeshwa kwa Wanajumuiya kujitolea muda wao na hivyo kuwa na uzito kupata muda na kwa sababu hii tumeona ni vyema kutoongeza majukumu mengine ila haya ambayo tuliyo nayo tujitahidi kuyaboresha. Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atupe uwezo wa kuisimamia dini yake na atupe msukumo na hima katika kufanya kazi hizi kwa ajili ya kupata ridhaa yake Subhaanahu Wata’ala na atujengee misimimamo thabiti katika kusimamia haki na kuitekeleza. |
|
|
 |
|
 |
|
|
|
|
 |
|
 |
|
|
Aya za Quran |
Displaying: Srh. Al-Qalam (68) Ayat 38 | | 68.38 . That ye shall indeed have all that ye choose?
[ Srh. Al-Qalam : 38 ] | |
|
Who's Online |
|
We have 6 guests online |
|
|
 |
|
 |
|